Menu

10. shirika la kazi

Kasi ya uandishi wa habari inaamriwa na kutokea kwa habari. Na habari haikomi. Uandishi wa habari hauna mapumziko. Ili kufanya kazi hii, waandishi wa habari wanapaswa kuwa na afya njema na usawazisho mzuri wa kazi na mapumziko, lazima wajifunze kufanya kazi kwa haraka na lazima wawe na utulivu wa akili. Iwe anafanya kazi mtu peke yake au katika chumba cha habari cha gazeti kubwa, waandishi wa habari inawabidi kupangilia kazi yao iendane na ufinyu wa muda.

NIDHAMU YA MTU  INAONESHA ANAVYOHESHIMU KAZI YA WENGINE

 1. Heshimu urefu wa habari.Habari ndefu kuliko ilivyotarajiwa ni kupoteza muda wa kila mmoja: mtu wa kuifupisha, mtu wa kuiandaa kupiga chapa, mtu wa kupiga chapa na mchapishaji.
 • Chukulia habari yako ya mwanzo kama rasimu, kisha isome tena, ukihakikisha kufuta habari yoyote isiyo na maana ili kuendana na ukubwa uliowekwa, kwa urefu wa karibu kabisa na jumla ya maneno.
 • Kufuta habari isiyo na maana inahusisha kuondoa chochote kile ambacho si muhimu kwa kujenga uelewa: vivumishi, vielezi, vibainishi vinavyojirudiarudia,kuweka viunganishi sawasawa, nk.
 • Ukitaka kupunguza maneno 15 na takribani herufi mia moja badala ya kuandika: “Majambazi wawili wenye sura za kutisha ambao hawakuweza kutambulika kutokana na kufunika vichwa vyao kwa vinyago vya kubana kama tahadhari, wamemteka Mark Mahela”, badala yake utaandika: “Mark Mahela ametekwa na watu wawili waliofunika nyuso zao”. Kuzingatia viwango mara zote huboresha kazi iliyofanyika.
 1. Heshimu mwisho wa kuwasilisha kazi.Kuchelewesha habari ni jambo linalotesa wote wanaohusika na husababisha: uhakiki dhaifu, masahihisho ya harakaharaka, hatari ya kuwa na makosa ya kimaudhui, ucheleweshaji uzalishaji na matatizo katika uchapishaji.
 • Jiaminishe kwamba kuwasilisha habari yako ndani ya muda uliowekwa ni muhimu zaidi kuliko hata habari yenyewe. Mwisho wa kuwasilisha habari unakaribia, kwa hiyo nitaandika yale mambo muhimu tu ya habari yangu. Mambo mengine naweza kuyaandika siku nyingine katika toleo jingine. Ni bora kuwasilisha habari fupi na ambayo haijakamilika kuliko kuwasilisha habari ndefu na iliyokamilika lakini ikiwa imechelewa.
 1. Heshimu wafanyakazi wenzako. Kufanya kazi katika timu si jambo rahisi pale timu hiyo inapojumuisha watu wanaojitegemea sana waliozoea kuandika peke yao. Hilo linahitaji sifa mahsusi: kujua namna ya kuwasikiliza wafanyakazi wenzako, kujua namna ya kubadilishana habari, kujua namna ya mchakato wa fikra za watu wengine na kujua jinsi ya kufikia makubaliano. Uzalishaji wa kila siku wa habari hauendani kabisa na kufanya mizaha. Inahitajika kugawana majukumu ya kila siku kwa ufasaha.
 • Zingatia kwamba malenga wazuri sana si lazima awe manjo mzuri. Awe ni mkurugenzi, mhariri mkuu, mhariri wa idara au mhariri msaidizi, waandishi wa habari wanaofanya kazi ya usimamizi lazima wajue kusimamia, kuhamasisha na kuongoza timu, na mara nyingine namna ya kukasimu baadhi ya majukumu yao. Hilo ni jambo ambalo mtu anaweza kujifunza.

Mbinu iliyothibitika: weka kanuni kwamba hakuna mwanatimu ya waandishi wa habari ambaye ndiye pekee mwenye haki ya kushika cheo alichonacho.

NIDHAMU YA PAMOJA HUTOA GAZETI BORA

Nidhamu binafsi ni jambo lisiloepukika kwa uzalishaji bora wa pamoja. Lakini si namna zote za kuongoza wandishi wa habari hutoa matokeo yanayofanana. Mbinu bora zaidi ni kumfanya mwandishi wa habari yeye mwenyewe amiliki kikamilifu kazi yake ya kila siku.

 • Shirika dogo

Ngazi mbili: moja inatoa maagizo, nyingine inayatekeleza. Mamlaka yote inashikiliwa na mwandishi mmoja, ambaye kwa kawaida ndiye mmiliki wa gazeti. Yeye ndiye mkurugenzi na mhariri mkuu, anaajiri waandishi wa habari wachache wenye uwezo mkubwa na kugawa majukumu kulingana na anavyoona inafaa.

Faida: timu nzuri, inayoshirikiana kwa karibu, isiyo na urasimu na yenye watu wanaosaidiana.
Hasara: uongozi kwa mtindo wa kueleana, hatari ya kufanya kazi kwa mazoea, nafasi finyu ya kupanda cheo, kukosekana kwa mada nyingi katika maudhui.

 • Shirika msonge

Ngazi nne: moja kwa Afisa Mtendaji Mkuu, nyingine ya kutoa maagizo, moja ya juu ya kuyatekeleza na moja ya chini ya kuyatekeleza. Wajibu umewekwa kwa mtu mmoja tu wa ngazi ya juu. Mwandishi wa habari mkuu anachagua mhariri wa habari ambaye naye anateua wasaidizi kadhaa ambao anawakabidhi uongozi wa idara zinazoundwa na waandishi wa habari wenye uwezo mbalimbali.

Faida: timu yenye utaratibu maalum, mshikamano, nidhamu na ufanisi.
Hasara: hatari kwamba madaraka yatatumika vibaya, mawazo yale yale, maudhui yale yale, ukosefu wa kugonganisha mawazo, uandishi wa habari usioeleweka vizuri msimamo wake.

 • Shirika la pembe tatu

Ngazi tatu: moja inahakikisha udhibiti, nyingine inatoa maagizo na ya tatu inayatekeleza. Mamlaka yamegawanywa. Afisa Mtendaji Mkuu na mhariri wa habari wanakasimu madaraka yao kwa wakuu wa idara ambao wako huru kuamua nani wamwajiri na nini wakiandike. Kila timu ya uhariri, inayoundwa na waandishi wa habari wabobezi au wenye uwezo mbalimbali, inafanya kazi kwa kujitegemea.

Faida: kuwa na habari nyingi, ushindani wenye tija wa ndani, utendaji wa hali ya juu, kiwango kikubwa cha utaalamu.
Hasara: kufanya mambo kwa siri, ubobezi uliopitiliza, ukosefu wa mawazo mtambuka, kujiona bora zaidi.

Dondoo muhimu: mifumo ni mizuri tu kulingana na watu wanaoiendesha.