SIFA SITA ZA UANDISHI MZURI WA HABARI ZA UCHUNGUZI:
- Swali zuri
Nyuma ya uchunguzi wowote mzuri, siku zote kuna swali la nyongeza. Mara nyingi, hili ni swali linaloweza kusahaulika ambalo mchunguzi makini atajiuliza pale atakapopata majibu ya maswali yote makuu, lakini ambalo wengi hawathubutu kujiuliza kwa kina kwa hofu ya kile linachoweza kuzua. Mara nyingi ni swali la “kwa nini” ya “namna gani” au “namna gani” ambayo umeitilia shaka, lakini huwezi kuliona kulingana na ukweli ulionao.
Hebu tuchukulie kwamba tayari nimepata majibu yote ya maswali niliyouliza kuhusu ujenzi wa makao makuu ya Benki ya Wafanyakazi katika eneo lenye ulinzi mkali kwenye kisiwa cha Sinde. Ninacho kile nachohitaji kuandika habari kamili kuhusu madhara ya mabadiliko haya, maisha mapya ya mmiliki maarufu wa benki, hali ya akili yake, mipango yake, na kadhalika. Ripoti yangu ya kipekee kuhusu wakazi wa kisiwani wasioridhishwa na ujenzi itakuwa ni kikolezo cha habari kuu niliyonayo. Naridhika na kile nilichofanikisha… Ilhali kuna swali la ziada linalosumbua akili yangu. Lakini ni swali zito kiasi cha kwamba mimi mwenyewe litaniacha na mshangao. Ni kwa namna gani Mark Mahela aliweza kujenga jengo kama lile katika eneo la hifadhi ya uoto wa asili? Aliwezaje kupata vibali muhimu? Ni halali kisheria? Na amewezaje kumudu gharama za ujenzi wa jengo kubwa kama hilo wakati inasemekana amefilisika? Nashangazwa na maswali hayo, lakini sijui namna ya kuyajibu. Yaani kuna vikwazo vingi sana…
- Chanzo
Waandishi wa habari za uchunguzi hujaribu kufukua habari zisizopatikana kirahisi kama ambavyo wanahistoria nao hutafiti kazi zao katika mazingira ya kutokuwa na taarifa za kutosha. Kupata chanzo, waandishi wa habari wanatumia mbinu zile zile kama wanahistoria: wanatafiti mada iliyowavutia, wanatafuta kumjua zaidi mkinzani, wanasoma kila kitu kilichoandikwa juu yake, wanatayarisha orodha ya mashuhuda wanaofahamika na wale wanaoweza kuwa mashuhuda, wananukuu tarehe muhimu na nyakati katika maisha binafsi na ya kikazi ya mkinzani, wanatayarisha orodha ya maswali yaliyojitokeza kutokana maswali ambayo hayajajibiwa… Kwa lugha nyingine, wanapambanua fumbo la kile wanachotaka kukipatia jibu.
Katika hili suala la Mark Mahela, haraka inaelekea dhihirika kwamba amepata msaada wa kifedha kutoka kwa mfanyabiashara mkubwa Rashid Pesamali, ambaye anamiliki shirika muhimu na ni mtu tajiri. Mmiliki huyo maarufu wa benki pia alifanya vikao kadhaa na Fatma Kijiko, Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Maeneo ya Hifadhi.
Hapa sasa kuna dondoo yako ya awali: tafiti zaidi kuhusu Fatma Kijiko, uhusiano wake na Mark Mahela, ni mara ngapi wamefanya vikao katika miezi ya hivi karibuni, ongea na rafiki zake wa karibu na familia yake kuhusu kuhamishwa kwa makao makuu ya Benki ya Wafanyakazi kwenye kisiwa cha Sinde, licha ya kwamba ni eneo la hifadhi ya uoto wa asili, nk.
- Kusuka tandabui
Pale waandishi wa habari wanapokuwa wanahistoria wa wakati uliopo, wanahitaji muda wa kufahamu mada yao, kuelewa wigo wake na kisha kuiandika. Wanachukua muda wote huo kwa sababu ni muhimu. Wanapiga hatua taratibu, wakianzia kipengele kimoja muhimu hadi kingine.
Watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii kama vile Rashid Pesamali au Fatma Kijiko wana washindani na maadui. Mashuhuda hawa kwa hakika watakuwa na mambo ya kusema kuhusu usaidizi ambao watakuwa wameutoa kwa mradi mkubwa wa Mark Mahela. Natayarisha orodha ya watu hawa na kutafuta taarifa zaidi, ambazo naweza kuzitumia kupata ushirikiano wao. Hawa ni watu nitakaokutana nao kwanza, kwa sababu watakuwa na utayari zaidi wa kuongea nami kuliko Fatma Kijiko mwenyewe, au familia yake na rafiki.
Waandishi wa habari wanaanzia mbali kusuka tandabui ya mada yao na kidogo kidogo wakielekea kwenye maswali makuu.
- Kuboresha tandabui
Mahojiano mara zote huzua maswali mapya.
Nikishajenga kuaminiwa, mashuhuda wangu wa mwanzo wananipa vyanzo vingine vya habari. Ingawa Mark Mahela alinufaika na usaidizi mkubwa kutoka kwa Rashid Pesamali, pia aliongeza utajiri wake kwa kununua makampuni kadhaa, ambayo baadhi yake yaliingia katika matatizo. Sipati shida ya kuwafanya wakurugenzi wa zamani wa makampuni haya waongee. Wananieleza kwa kina ni namna gani mmiliki huyu maarufu wa benki anavyoendesha mambo yake. Pia nagundua kwamba amemfahamu Fatma Kijiko tangu utotoni kwa vile walisoma pamoja. Pia amekuwa mshauri wa muda mrefu wa Benki ya Wafanyakazi, lakini kwa kutumia jina la usichana… Taarifa inaanza kunoga.
Sasa unafika wakati kwa mwandishi wa habari za uchunguzi kuchambua, kufumbua na kunyoosha taarifa zilizokusanywa lakini akiwa bado anaiambaa-ambaa habari yake. Anathibitisha takwimu, anakusanya nyaraka, anatafiti upya ukweli wa maelezo ya mashuhuda na anatayarisha mpango kazi.
- Mkakati wa buibui.
Wakishalizunguka windo lao, waandishi wa habari za uchunguzi hushambulia moja kwa moja, bila ya kusita, wakiwa salama kwa kufahamu kwamba wana zana zote wanazohitaji. Kinachobakia ni kukamilisha kazi yao kwa kumtaka mlengwa kutoa maelezo ya ukweli waliougundua. Hili ni jukumu la kimaadili la mwandishi wa habari: ikiwa wataandika habari kumhusu mtu, lazima wampe nafasi ya kujieleza. Lakini, unaweza kunasa inzi wengi zaidi kwa asali kuliko kwa siki…
Kwa hiyo, naomba kufanya mahojiano na Mark Mahela. Vyema zaidi, nafanya hivyo kwa maandishi, kwa kutumia maneno kwa makini na kirafiki, kuonesha kwamba siegemei upande wowote. Lakini sioneshi kabisa madhumuni yangu halisi ili nisimwogopeshe. Akikubali kukutana nami, hapana shaka nitajumuisha majibu yake katika habari yangu. Ikiwa atakataa, hilo pia litajumuishwa, ili kwamba wasomaji wangu wajue kwamba nilitenda kwa nia njema.
Mwandishi wa habari za uchunguzi lazima awe muwazi sana katika kazi yake kuonesha ni namna gani anavyoheshimu ukweli na wasomaji wake.
- Hoja isiyopingika.
Uchunguzi uliofanyika vizuri ni rahisi kuandika habari yake. Ukweli, maelezo ya mashuhuda na ushahidi unaunganika kuunda mtiririko wa kimantiki, sawa sawa na kupata jibu la fumbo la hesabu.
Ili kunogesha habari yao, waandishi wa habari huongeza baadhi ya mambo waliyoyaona au kuyasikia kama ushahidi wao, lakini mambo haya ni kama vinogesho tu. Chochote kinachoweza kufanya wasomaji wao watoke kwenye mada kuu kinawekwa kando. Maoni binafsi hayana nafasi hapa (isipokuwa, hapa na pale, katika hitimisho au maoni ya mhariri) kwa sababu ukweli unajieleza.
Jambo muhimu ni namna gani utakavyoelezea hoja yako kuu bila ya kumung’unya maneno, ambayo lazima yaunge mkono kicha cha habari yako ya kichunguzi na hitimisho lake.
HABARI YOYOTE YA UCHUNGUZI INAYOFANYWA NA ZAIDI YA MTU MMOJA INAHITAJI KURATIBIWA
Baadhi ya habari za uchunguzi zinahitaji kuziandika kutokea pande mbalimbali. Kufanya kazi mtu mmoja, hata awe ni mwandishi wa habari mahiri anaweza asifanikiwe kupata habari zote, hasa pale anapofanya uchunguzi mkubwa zaidi ili kufuatilia vyanzo vyote. Katika hali hii, kushirikisha waandishi wa habari wengi katika uchunguzi ndiyo mbinu bora zaidi. Katika mfano wetu, tungeweza kuigawa kazi katika sehemu tatu, kati ya waandishi maalum wawili wa habari za mazingira na fedha, na mwandishi wa kawaida wa habari kushughulikia mambo yanayoonekana na kusikika uwandani. Ugumu wa mbinu hii uko katika kudumisha usimamizi wa kazi na kisha kuiandika. Uongozi madhubuti na mratibu wa jumla ni muhimu kuwepo.
UCHUNGUZI WOWOTE UNA MAPUNGUFU YAKE.
Mafanikio ya chunguzi za uandishi wa habari wakati mwingine hutegemea uwezo wa mwandishi wa habari za uchunguzi kutoa maelezo au kuficha mawazo yake. Lazima athibitishe uwezo wake wa kuibua ukweli uliofichwa. Kutafuta ukweli kwa maslahi ya umma unawahalalishia kuwa watukutu. Lakini kazi hii kwa niaba ya umma isichanganywe na haja ya kukidhi matamanio binafsi au kiu binafsi ya kulipa kisasi. Unyofu katika uchunguzi wowote humtaka mwandishi wa habari kuwa muwazi kuhusu kinachomhamasisha. Hatuchunguzi kwa ajili ya tamaa zetu binafsi, lakini kwa sababu jamii ina haki ya kujua ukweli. Waandishi wa habari za uchunguzi si maafisa wa polisi au mahakimu; hatugeukii kutumia mbinu ya udanganyifu.