Menu

23. “Huduma kwa Wateja”

Gazeti likishachapishwa, mwandishi wa habari lazima awajibike kwa maudhui yake. Ni kawaida, na hata ni jambo lenye tija, kwa habari ya mwandishi wa habari kuwa jambo la kukosolewa na wenzake na wasomaji. Kukua kwa njia za mawasiliano ina maana kwamba waandishi wa habari lazima wajumuishe majadiliano ya kudumu na ya wazi kwa wale wanaoamini ni namna gani wanavyotenda kazi yao.

KUWAJIBIKA KWA WASOMAJI

Popote wanapopata nafasi ya kuweza kufanya kazi yao kama “wasema ukweli” kwa uhuru kamili, katika jina la haki ya watu ya kupata habari za kweli, waandishi wa habari kamwe hawaachi kuwawajibisha wengine: wanasiasa, mamlaka za umma, serikali, mashirika, vyama, makampuni, vilabu, nk. Kwa upande mwingine, ni kawaida kwa waandishi wa habari kuwajibika kwa wengine kwa kazi yao ya kiweledi na wanachokiandika.

KUJIBU BARUA ZA WASOMAJI SI MZIGO, BALI NI UPENDELEO

Wasomaji makini, kama mteja yeyote yule, kama ilivyo ada, daima wako sahihi. Hata, na hasa, wakisoma habari kimakosa, wakisoma vibaya nia ya mwandishi, wakielewa vibaya au kutafsiri vibaya habari, wanayo haki ya kutarajia kutendewa kwa uungwana na heshima kutoka kwa waandishi wa habari ambao wanahoji mambo wanayoyachapisha. Uzoefu unaonesha kwamba ikiwa waandishi wa habari watakubali kukosolewa na kuitikia kwa nia njema, wasomaji ni waelewa, hata wapenda amani, kiasi cha kukubali, wakati mwingine, kwamba “hawakuelewa”. Kuzungumza na wasomaji daima huongeza thamani kwenye uandishi wa habari na, kwa waandishi wa habari, ni somo kwa ajili ya tafakuri. Njia rahisi zaidi ya kupata wasomaji unapofanya biashara ya gazeti ni kuongeza nafasi maalum kwa ajili ya barua za wasomaji.

HAKI YA KUPEWA MAJIBU NI HAKI YA MSINGI

Kwa haki zote walizonazo wasomaji, haki ya kupewa majibu ya kumkabili mtu binafsi ndiyo muhimu zaidi. Hakuna kitu, si sheria wala hoja, kinachopaswa kuzuia uchapishaji wa majibu ya msomaji aliyenukuliwa au kutajwa katika habari. Majibu kama hayo lazima, bila shaka, yawiane na habari husika. Urefu wake, maudhui, lugha na muundo unaweza kujadiliwa, kuzungumzika na kujadiliana. Ukweli kwamba ulishambuliwa vikali hautoi haki ya kujibu mapigo kwa ukali. Hata hivyo, katika kila hali, hakuna kitu na hakuna mtu anayepaswa kuzuia uchapishaji wa “haki ya kujibu” inayodaiwa kihalali. Hakuna jambo linalomzuia mwandishi wa habari kujadili kwa uhuru jambo hilo hilo na wasomaji wengine. Hata hivyo, tahadhari ichukuliwe, kwa vile wasomaji wengi wanajua tofauti kati ya nia njema na nia ovu…

KUSAHIHISHA MAKOSA NI LAZIMA 

Hakuna ushahidi bora zaidi wa nia njema kwa upande wa waandishi wa habari, machoni pa wasomaji wao, zaidi ya kusahihisha makosa yao bila kutakiwa kufanya hivyo. Gazeti lisilochapisha masahihisho si gazeti adilifu. Waandishi wa habari wote wakati mwingine wanakosea katika uandishi wao. Ingawa makosa mengine hayana madhara, makosa mengine yanaweza kuwa na madhara makubwa. Masahihisho ya lazima ni moja ya kanuni kuu zinazoheshimiwa na magezeti makubwa. Kuifanya “huduma” hii imfikie kirahisi msomaji, masahihisho kwa kawaida huchapishwa kwenye eneo lile lile la ukurasa ule ule.

***

Kesho, katika sehemu hii, nitachapisha masahihisho yafuatayo, kwa sentensi mbili zilizo wazi kadri iwezekanavyo, bila ya kutoa visingizio: “Kinyume na kile tulichokiandika kwenye ripoti yetu kuhusu wakazi wa kisiwani wasiofurahishwa na  kuhamishiwa makao makuu ya Benki ya Wafanyakazi kisiwani Sinde, jana, katika ukurasa wa 3, si meya Kamba Mchago, aliyetoa kibali cha ujenzi kwa Mark Mahela, bali mmoja wa wasaidizi wake, Kambi Kichogo. Tunawaomba wasomaji wetu mtuwie radhi kwa mkanganyiko huo.” 

KUMTAMBULISHA MSULUHISHI? NDIO, LAKINI…

Wasomaji wamekuwa muhimu sana kwa magazeti kiasi cha kwamba magazeti mengi sasa yanaajiri mtu “mwenye sifa stahiki” (“msimamizi wa maadili” au “msuluhishi”) kwa jukumu la kuwa na mjadala wa wazi na wasomaji wao na kujibu malalamiko yao kuhusu maudhui ya habari. Barua za wasomaji kwa ujumla zinatoa nyenzo za “zinazoelimisha” kwa ajili ya kujikosoa mara moja kwa wiki. Hata hivyo, shauku hii ya kuwa na uwazi haitoi matokeo yale yale kila mahali. Inategemea sana na “sifa” za mtu “mwenye sifa stahiki” aliyechaguliwa kwa kazi hii ya msuluhishi au mpatanishi. Mtu huyo lazima awe aliwahi kuwa mwandishi wa habari, na lazima ajue mbinu zote za kazi, ili aifanye kazi yake kwa uhalali stahiki.