Menu

19. proofreading

Unapoandika ni jambo jema kupitia upya habari yako. Ukiwa mwandishi hiyo ni lazima. Lakini haitoshi tu kupitia upya kazi yako kuhakikisha kwamba unachowapa wasomaji hakina makosa. Kila mwandishi ana kasoro na madhaifu yake. Katika uandishi wa habari wa kiweledi, kupitia upya habari na mtu mwingine ni jambo la lazima.

KUPITIA UPYA HABARI NI JAMBO LA KIMAADILI: 
HABARI HAIPASWI KUCHAPISHWA KABLA YA KUPITIWA UPYA NA, IKIBIDI, KUSAHIHISHWA NA MTU MWINGINE KANDO YA MWANDISHI WAKE.

Wataalamu wa kupitia upya nakala ni kizazi kinachopotea. Hii ni aibu kubwa kwa vile kompyuta kamwe hazitakuwa mbadala wa jicho la mpitiaji upya makini. Siku hizi, ni juu ya waandishi wa habari wenyewe kwenye chumba cha habari kusaidiana kupitia upya na kusahihisha habari kabla ya uchapishaji. Hakuna upendeleo katika jambo hili: bila kujali mwandishi, awe ni mwandishi mwanafunzi au mkurugenzi wa gazeti, hakuna habari inayopaswa kuchapishwa kabla haijapitiwa upya kwa umakini.

Mnyororo wa uzalishaji ambao unaangalia ubora wa habari una ngazi mbili za upitiaji upya: kwanza, kule habari ilikoandikwa (kitengo au idara) na kisha, kule ambako inahakikiwa kabla ya kuchapwa (mhariri msanifu mkuu au kitengo cha wasomaji upya). Utaratibu unaofaa zaidi ni ule unaogawa kazi ya upitiaji upya kwa wahariri wa idara na wasaidizi wao.

UPITIAJI UPYA NDIYO FURSA YA MWISHO YA KUIONGEZA THAMANI HABARI.

Upitiaji upya ni kusahihisha makosa yoyote ya kisarufi na makosa ya kuchapa, kusahihisha maeneo yoyote yenye utata au kutumia maneno mengi bure, kuandika upya aya mbaya, kuhakikisha herufi kubwa zinatumika ipasavyo, nk. Kwa mfano: “Mark Mahela atatua (si apata ufumbuzi wa) matatizo yake ya kifedha wakati katibu muhtasi wake afidia ukosefu wa kahawa (na si kukosekana kwa…) kwa kunywa soda. Mmiliki wa benki anapaswa (si alikuwa anapaswa) kuwashawishi wanahisa lakini wako makini sana kiasi cha kutorudia makosa ya nyuma (kutorudia tu badala ya “kutorudia tena”, ambayo ingekuwa maneno mengi bure), nk.

Upitiaji upya huboresha habari kwa kuondoa sentensi zote zilizoandikwa vibaya, kuhakikisha kanuni za uakifishaji zimetumika kwa usahihi, kuondoa mawazo potofu, au kuondoa maneno yanayotumika bila umakini. Kwa mfano, tunapaswa kuacha “kuchora mstari”, “tugange yajayo”, “funika kombe mwanaharamu apite”, au “acha liende”! Na tuache kutumia vibaya mabano na alama za mshangao! Na inapokuja kwenye nukta endelezi daima zinatumia nukta tatu tu…

Upitiaji upya huboresha habari kwa kuondoa virai visivyofaa na kujirudia rudia, kwa kuweka maneno sahihi badala ya yasiyofaa, kwa kutumia maneno ya maana kuliko yasiyo na maana, na kuingia kwa kina katika utajiri wa lugha yetu kubadilisha uandishi wa kutumia mawazo potofu kuwa habari ya kupendeza. Kwa mfano: “mahari” si sawa na “mahali”, “fahari” kwa namna yoyote ile haimaanishi “fahali”, “ajari” si “ajali”, na “jinsi” kamwe “si jinsia” katika mikono ya mwandishi.

Hitimisho: kila mwandishi wa habari anahitaji kuwa na kamusi pembeni yake. Ni kitabu muhimu kwa matumizi ya kila siku linapokuja suala la upitiaji upya habari.

Katika chumba cha habari kunapaswa kuwa na kamusi ya nomino za kawaida, kamusi ya nomino kuu, kamusi ya nukuu, kamusi ya visawa na mwongozo wa changamoto za sarufi na sintaksia wakati wote. Linapokuja suala la matumizi ya lugha Kamusi ya Kiswahili Sanifu inayo mifano mingi ya namna maneno yanavyotumika katika Kiswahili.
Waandishi mra zote hunufaika kitaaluma kutokana na mapitio ya kazi zao, na hukubali masahihisho kwa hiyari. Hata hivyo, wapitiaji upya wanapaswa kutambua hisia za waandishi au umimi: maoni kuhusu makosa yanapaswa kufanyika kwa heshima, bila ya kejeli, na ana kwa ana katika faragha.

KUPITIA UPYA HABARI SI KUTAFSIRI UPYA.

Yawezekana, hapa shaka, kukawa na wakati ambapo mpitiaji upya anahoji maudhui, kuliko tu mtindo wa uandishi. Udhaifu wa maelezo ya shuhuda au maoni husika yanaweza kumfanya mhariri mkuu kuhoji ubora wa uchambuzi au unyambuaji wa habari. Hilo husababisha hali tete ambalo linapaswa kushughulikiwa kwa tahadhari; zaidi ya yote, upitiaji upya hauhusu kutoa tafsiri mpya ya kazi ya mwandishi. Masahihisho yaliyofanyika kuboresha habari hayapaswi kupotosha maana ya habari au mtindo wa mwandishi. Kwa vile uandishi wa habari ni kazi ya kushirikiana, uondoaji wa vipengele au uandikaji upya unapaswa kujadiliwa na kuratibiwa. Inabidi kuwe na makubaliano kati ya waandishi na wakuu wao wa kazi.
Ikiwa kila mmoja atatenda kwa nia njema, mchakato wa marekebisho utaenda vizuri. Mabadiliko yanayolazimishwa kutoka juu kamwe hayana tija.

FAIDA YA UPITIAJI UPYA HUBADILIKA MARA KWA MARA…

Lugha zote zinakua. Katika miaka 20 iliyopita, lugha ya Kiswahili imebadilika sana. Na kwa kuwa Kiswahili ni lugha ya kinahau, hakuna tahadhari inayotolewa kuhusu mabadiliko hayo. Hata hivyo, mwandishi wa habari mzuri hutafuta na kufuata mabadiliko hayo. Na hujifunza kuyatumia kikamilifu!