Menu

07. uongozi wa habari

Kwa mwandishi wa habari, habari kubwa ni ile habari yenye umuhimu kwa wasomaji wa gazeti. Kipaumbele cha habari kinaamriwa na wigo ambao mwandishi wa habari anafanyia kazi kama mzalishaji habari. Hata hivyo, bila kujali ni gazeti gani linahusika, habari inayowafurahisha baadhi ya wasomaji si lazima pia iwafurahishe wengine. Mipaka ya vipaumbele vya habari haiokenani kirahisi. Kipaumbele hutofautiana kati ya gazeti na gazeti.

KUNA KANUNI TANO KUU:

Kanuni ya ukaribu wa kijiografia: kile kinachotokea nyumbani ni muhimu zaidi kuliko kile kinachotokea kwingineko. Hii ndiyo sababu kuu ya kuwepo kwa gazeti mahalia. Kutekwa  kwa Mark Mahela ni tukio kubwa kwa Watanzania, lakini ni la mbali sana kwa watu wa Australia.

Kanuni ya ukaribu wa muda: kile kinachotokea leo ni muhimu zaidi kuliko kile kilichotokea jana. Hii ndiyo sababu kuu ya kuwepo kwa gazeti la kila siku. Gazeti la “Habari Leo Dar es Salaam” litatoa kipaumbele kwa habari ya kina ya kutekwa kwa Mark Mahela kwenye makao makuu ya Benki ya Wafanyakazi iliyoko Mtaa wa Ngawira.

Kanuni ya ukaribu wa kihisia: kile kinachogusa mapenzi ya wasomaji ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote. Hii ndiyo sababu kuu ya magazeti ya udaku. Baadhi ya wasomaji watapenda zaidi kujua maisha binafsi ya tajiri wa kutupwa Mark Mahela kuliko maamuzi yake ya kimkakati kwenye benki.  “Gazeti la Ubuyu Dar es Salaam” litatoa kipaumbele kwa mahojiano na mkewe.

Kanuni ya ukaribu wa utendaji: habari rahisi ni rahisi kupatikana kuliko habari ngumu. Hii ndiyo sababu kuu ya kuwepo kwa magazeti huru. Gazeti la “Mtafiti Dar es Salaam” litachapisha mfululizo wa makala za vielelezo kuhusu Benki ya Wafanyakazi: ramani ya matawi yake ya kikanda na kimataifa, idadi ya wafanyakazi, takwimu za ukubwa wa biashara yake, nk.

Kanuni ya ukaribu wa kimatumizi: ukweli mahsusi unavutia zaidi kuliko ukweli dhahania. Hii ndiyo sababu kuu ya kuwepo magazeti yanayoweka mkazo katika huduma.  Gazei la “Nyuki Dar es Salaam” litatoa ukurasa wake wa mbele kwa masuala ya ulinzi.

***

Habari muhimu zaidi ni ile ambayo huhusisha sehemu kubwa ya kanuni hizo hapo juu. Kama una mashaka, jadili jambo hili kwenye chumba cha habari: ni habari gani kubwa zaidi leo kwa idadi kubwa ya wasomaji wetu? Kugonganisha mawazo hurahisisha kazi ya kuchagua kipaumbele na hasa huamua mwonekano wa ukurasa wa mbele.

KUNA MPANGILIO WA VIPAUMBELE

Ingawa habari ni bidhaa, si bidhaa ya kawaida: ni bidhaa ambayo uhai wake sokoni unadumu muda mfupi sana. Kila timu ya uhariri inaweza kuweka vipaumbele vyake kulingana na mkazo wao na kwa msingi wa vipaumbele vya kazi yao. Inaweza kufanya hivyo kwa kuchagua nini kipewe msisitizo kwenye mada za kuandikwa ili kuunganisha mapenzi yake na yale ya wasomaji.

Je, Mark Mahela ametekwa?  Gazeti la “Muungano wa Mabenki” moja kwa moja litachukua upande wa wasomaji wake kwa kuchapisha toleo maalum. Kichwa cha habari kikubwa ukurasa wa mbele: “Tahadhari ya kutekwa!” Kiwiliwili cha gazeti: maelezo ya kina ya tukio yanayoandikwa katika matoleo mawili. 1. Mateka (wasifu wa Mark Mahela, muhtasari wa maisha yake ya kikazi, uchambuzi wa hali ya Benki ya Wafanyakazi, maelezo ya mashuhuda, nk.) 2. Matokeo (habari inayoelezea kwa kina kuwatuliza wanahisa, mahojiano na mkewe, ushauri halisia kwa wamiliki wa mabenki, maoni ya mhariri, nk.)

UFUMBUZI ULIO BORA: MGAWANYO WA VIPAUMBELE

Kutoa majibu bora zaidi kwa maswali, swali linapaswa kugawanywa katika maswali madogo madogo:

  • Nini kinawavutia wasomaji wanaopenda siasa za ndani?
  • Nini kinawavutia wasomaji wanaopenda siasa za nje?
  • Nini kinawavutia wasomaji wanaopenda mambo ya kiuchumi na kijamii?
  • Nini kinawavutia wasomaji wanaopenda habari za kitamaduni na michezo?

nk.

Mada zinashughulikiwa ipasavyo.

Ikiwa una mashaka, weka kipaumbele kwenye ukweli wako. Mpe msomaji zana anazohitaji ili kufikia maoni yake mwenyewe.

Mfano wa kipaumbele cha habari kwenye ukurasa wa habari wa kawaida:

  1. Habari ya kina ya ukweli (habari au taarifa).
  2. Maelezo ya mashuhuda kuhusiana na matukio (taarifa au “sauti ya watu”).
  3. Mwitikio kwa matukio hayo (taarifa au habari za mashirika ya habari).
  4. Maswali yanayoibuliwa na matukio hayo (uchambuzi)
  5. Maoni ya jumla (maoni ya mhariri)