Menu

06. Comments

Waandishi wa habari nao ni binadamu tu. Hulka yao, mapenzi, elimu, hisia, imani na mitizamo vyote hivyo huchangia kwa namna wanavyouona ukweli, hata pale wanapochukua kila tahadhari kutokuwa na upande wowote. Namna ya hakika ya waandishi wa habari kuthibitisha uadilifu wao kitaaluma kwa wasomaji wao, ni kuhakikisha, kamwe kutochanganya ukweli na maoni.

EPUKA KUTOA HUKUMU ZA CHINI CHINI

Hata habari za ukweli sana haziwezi kuepuka kuchanganya maoni na ukweli. Inachukua nomino moja tu, kitenzi au kivumishi katika simulizi, ama iwe imetumika kwa makusubi au bila kutafakari sana, kumfanya msomaji achukue uamuzi kuhusu tafsiri fulani.

Kuandika “Mtaalamu wa Masuala ya Benki Mark Mahela…” si sawa na kuandika “Mwekezaji kwenye Soko la Hisa Mark Mahela…”. Kusema kwamba Mark Mahela ni mtaalamu wa masuala ya benki ni kueleza ukweli mtupu. Kumwita mwekezaji kwenye soko la hisa ni kufikia uamuzi wa kuchanganya ukweli na maoni.

Kuchagua maneno sahihi ni muhimu sana.

Daima hakikisha unatumia neno sahihi katika simulizi. Neno sahihi ni lile neno lisilo na madhumuni yaliyofichika.

TENGANISHA MAONI YA KUHISI

Mwandishi wa habari yeyote anayeipenda kazi yake anatetea uhuru wa kujieleza. Anaidai kwa ajili ya wengine, kwa ahiyo ni kawaida kwamba wao ndiyo wawe wa kwanza kufanya hivyo. Kuhusu wasomaji wa gazeti, wana haki ya kutegemea kwamba mwandishi wa habari anayewapa habari atachagia nao kwa uaminifu kabisa mtazamo wake wa mambo yanayotokea kila siku. Makala ya maoni ni aina nyingine ya kawaida ya uandishi wa habari. Hata hivyo, mwandishi wa habari anayetetea haki si mwanaharakati kwa maana ya kisiasa. Kuna njia moja tu ya kuhakikisha upashaji habari wa uadilifu: kutenganisha uandikaji ukweli dhidi ya kutoa maoni. Tenganisha mambo hayo mawili kwenye ukurasa. Kiuchapaji: andika habari mbili, moja inayohusu ukweli na nyingine inayotoa maoni ya ukweli huo. Kimwonekano: tumia fonti na aina ya uchapaji tofauti kwa habari hizo mbili. Koleza tofauti kwenye mpangilio: andika ukweli kwanza, ukifuatiwa na makala ya maoni; tumia kichwa cha habari kwa ukweli na kichwa cha habari kidogo kwa maoni.

Mpangilio wa makala ya maoni ni muhimu sana.

Makala ya maoni ni insha kuhusu simulizi ya mambo ya ukweli. Hata hivyo, si isha zote zina matokeo sawa. Hivyo ndivyo pia ilivyo kwa makala ya maoni: baadhi ya makala za maoni ni za kina, wakati nyingine ni za ukosoaji.

AINA TATU ZA MAKALA ZA MAONI

Kwa aina ya maoni mafupi, uandishi wa maoni unatumia zaidi utani kidogo au maneno makali kwenye makala ya maoni. Kadri makala ya maoni inavyokuwa fupi zaidi, ndivyo inavyokuwa na uzito zaidi: “Asubuhi ya siku hiyo, Mark Mahela alikuwa amewatangazia wafanyakazi wake kwamba watalazimika kukaza mikanda. Kwa hiyo kwa nini na yeye asikubali kulipa zaidi…?” 

Kwa aina ya maoni marefu zaidi, maoni ya mhariri ni njia bora zaidi kuliko aina nyingine mbili za makala za maoni: inampa msomaji hoja au msimamo.

Maoni changanuzi ya mhariri ni makala yenye muundo thabiti sana; aya yake ya kwanza inavutia na sentensi yake ya mwisho inapigilia msumari: “Akisha punguza wafanyakazi zaidi ili kuzalisha faida zaidi, Mark Mahela aliishia kujiweka hatarini yeye mwenyewe: siku chache tu kabla ya kutekwa nyara alikataa kusikiliza ushauri na akaamua kuwaachisha kazi timu nzima ya walinzi waliokuwa na jukumu la kumlinda. Jana tu, alitangaza uamuzi wake, ambao  wachunguzi wengi waliona hapakuwa na sababu ya kupunguza wafanyakazi wa benki kwa theluthi moja. Hapana shaka wafanyakazi wake wanashangilia kisirisiri kutekwa kwake: hatimaye ilikuwa tu itokee!” 

Maoni ya mhariri yenye msisimko yanaamsha hisia. Yanatoa zaidi msimamo kuliko kujenga hoja: “Kwa Mark Mahela milioni kadhaa ni kitu gani? Fikiria wafanyakazi aliowaachisha kazi!” 

MWANDISHI NA GAZETI WANAWEZA KUWAJIBISHWA KUTOKANA NA MAONI YA MHARIRI

Maoni ya mhariri daima yanakuwa na saini ya mwandishi wake juu au chini ili kuhakikisha uwazi na heshima kwa msomaji. Wajibu wa moja kwa moja kwa maudhui ni wa mwandishi; hata hivyo, wakurugenzi wa gazeti wenye dhamana ya uchapishaji wake nao pia wanawajibika kwa njia moja au nyingine.

Ikiwa wahariri wawili katika chumba cha habari wana maoni tofauti ambayo hawawezi kukubaliana linapokuja suala la kuandika makala ya maoni, hakuna kinachozuia gazeti kuchapisha maoni ya mhariri mawili kwa pamoja yanayounga mkono mitizamo tofauti. Jambo hilo litafurahiwa na msomaji.

Maoni ya mhariri yasiyokuwa na saini daima huelezea msimamo wa gazeti linaloyachapisha na kwa hiyo moja kwa moja ni wajibu wa wakurugenzi wa gazeti hilo.