Menu

17. kuandika

Kuandika habari ni kuandika kwa ufasaha. Hueleweka na, ni kwa ufupi. Huenda moja kwa moja kwenye mada. Hauna muda wa kupoteza. Hata hivyo lazima uwe sahihi sawa na uandishi wa masuala ya sayansi. Unatumia lugha rahisi ili uweze kueleweka na kila mmoja. Lakini pia unaweza kuwa wa kuvutia kama fasihi. Unatofautiana kulingana na aina zake za kueleza mambo. Kwa kifupi, kuandika habari kuna ukomo wake.

SWALI LA KWANZA: NATAKA KUSEMA NINI?

Unaweza kuandika vizuri ikiwa tu una fikra sahihi ya kile unachotaka kukiandika. Bila ya kujali aina ya uandishi unaotaka kuutumia kuelezea unachotaka kuandika, mwandishi wa habari anapaswa kuzingatia mambo muhimu, ujumbe mfupi lakini wa kujitosheleza ambao unauelezea kwa ufanisi katika mistari ya mwanzo kabisa ya habari yako.

Kwa mfano, katika habari: “Maisha katika kisiwa chetu kidogo tulivu yamegeuka jinamizi,” alalamika Mwenda Ngamani, mwenyekiti wa chama cha wakazi wa kisiwani wasioridhishwa na ujenzi, akiwa anaangalia bandari ya Sinde. Hapa ndiyo eneo lile lile ambapo, miezi mitatu iliyopita, Mark Mahela alijitambulisha kwa mara ya kwanza. Akiwa bado na machungu aliyopata baada ya kutekwa Mtaa wa Ngawira, aliamua kwamba hataacha tena usalama wake kuwa jambo la majaliwa.  Na hivyo ujenzi wa makao makuu ya benki yake, ambayo itaamishiwa Sinde mapema iwezekanavyo, ulianza. Mmiliki huyu maarufu wa benki kwa sasa hajui, lakini wakazi wa kisiwani hapo wana mpango wa kufungua malalamiko dhidi ya mradi wake…

Kisha elezea, kadri habari yako inavyoendelea, uwezekano wa madhara ya mgongano huu.

MASWALI MAWILI MUHIMU: 
NI NANI NAYEMSIMULIA HILI NA NI NAMNA GANI NILISEME?

  • Waandishi wa habari wanaandikia wasomaji wanaofahamika. Wanaandika ili kuwahudumia wasomajiwao . Lakini magazeti yote hayana wasomaji sawa. Waandishi wa habari wabobezi wanaandika kwa kuweka maanani mahitaji ya wasomaji wao. Ikiwa wanaandikia wasomaji vijana, kwa mfano, wanachukua nafasi ya mwalimu. Ikiwa wanaandikia wasomi, wanachukua nafsi ya mtaalamu. Waandishi wa habari hawajiandikii wao wenyewe, wanaandikia wengine. Wakati wakiandika kwa kuwafikiria wasomaji wao kwa ujumla, bado wanatilia maanani kwamba wanamwandikia kila msomaji binafsi. Wanaandika kwa lugha rahisi, ambayo inaeleweka na watu wote, kwa kutumia sentensi fupi zenye maneno sahihi tu, lakini wakiepuka lugha ya kupamba. Uandishi wao unatiririka haraka. Mdundo wake unaakisi hali ya sasa, uharaka wa habari yenyewe. Kutumia lugha rahisi ndiyo nguvu yake. Huwezesha kupata maelezo mengi kwa maneno machache tu: “Suti yake imechanika. Moshi unafuka kutoka kwenye viatu vyake vya ngozi. Anapiga hatua chache, magoti yakimtetemeka, na anatoka kwenye jengo, na kutorudi kamwe. Mark Mahela, akiwa ameshtushwa na mlipuko kwenye jengo lake lenye usalama wa hali ya juu, anaondoka kisiwa cha Sinde na kutorudi tena…“.

TUMEKUPA DOKEZO: FURAHIA UANDISHI WAKO.

Kuandika habari kuna kanuni zake, lakini si kwamba uko kimazoea. Huakisi maisha, katika uhalisia wake wote. Waandishi wa habari wachanga wanaotamani kuiga uandishi wa waandishi wakongwe wanafanya kosa. Kuandika habari, kwa bahati nzuri, hauna muundo unaofanana. Jambo jema kwa wasomaji! Ingekuwa hivyo, habari zingekuwa za kufanana sana kiasi kwamba wasomaji wangeyachoka magazeti. Mwandishi wa habari anahitaji kuibua mtindo wake mwenyewe, kuumiliki na kufanya uandishi wake kuwa wa kipekee. Wanafikia hapo kwa kufurahia kuandika kila siku. Ni suala la kujitahidi kufanya uandishi wako uwe wa kwako, au kutafuta namna ya kuelezea taswira, sauti na harufu ambayo ni ya kipekee kwako. Waandishi wa habari hujifunza kuandika habari sawa na wanavyopumua, kwa kucheza na tamathali za semi, kutoa mdundo na uhai kwa namna mawazo yao, maneno yao na taswira zao zinavyopangiliwa.

CHEZA NA MAANA YA MANENO:

  • Tafuta mifananisho stahiki.Acha mawazo yako yawe huru kutoa milinganisho sahihi. Hakuna kinachozidi taswira linapokuja suala la kupamba habari yako.  Kisiwani Sinde, jengo lenye usalama wa hali ya juu la Mark Mahela lilipuka? Linaonekanaje, mawe yakiwa yametapakaa ardhini? Taswira ni ya papo hapo: “Baada ya ujenzi kukamilika, kazi ya Mark Mahela imegeuzwa gofu…”.
  • Huisha mawazo dhahania.Kwa mfano, “Polisi kufanya upelelezi” chini ya jicho kali la “Jamhuri kuwasaka wahalifu…”! Lakini kuwa makini: ingawa mifananisho ni mbinu inayotumika sana katika uandishi wa habari, usipendelee sana kuitumia; hiyo ni kinyume kabisa cha kuandika kwa lugha rahisi.
  • Tengeneza aina mpya ya watu.Badili nomino za kipekee kuwa nomino za kawaida: “Kuanzia sasa na kuendelea, watu watamzungumzia mmiliki wa benki aliye matatani kama ‘Mahela-hela’…”
  • Tumia tafsida.Sema kidogo kumaanisha jambo kubwa zaidi: “Mark Mahela hataweza kuficha tena jambo lolote hivi karibuni…”.
  • Tumia kejeli. Kwa mfano, kwa kuelezea dhana kwa kutumia kinyume chake.

CHEZA NA MATUMIZI YA MANENO.

  • Lundika maneno.Endelea kidogo kidogo. “Kwa heri noti, dhahabu, hazina, maajabu!…  Hii inatengeneza shauku katika uandishi wako.
  • Tumia lugha ya mkazo.Ipe habari yako mdundo kwa kurudia neno la mwisho la aya katika mwanzo wa aya inayofuata: “Mark Mahela alikuwa kwenye ngazi. Ngazi zilikuwa na mteremko mkali…”. Au rudia neno hilo hilo la mwanzoni katikati ya aya hiyo hiyo: “Mark Mahela alikuwa kwenye ngazi, Mark Mahela alikuwa na haraka…”. Mchakato huu pia unaruhusu kuboresha habari: “Kwa vile Mark Mahela alikuwa na haraka, kwa vile ngazi zilikuwa na mteremko mkali, alipojikwaa…”, nk.
  • Ivike habari yako “mfano wa kioo cha kujiangalia”Kwa mfano, fanya hitimisho lako kuendana na ufunguzi wako. “Suti yake imechanika… Suti yake imetupwa…”. Au jizuie ili kusisitiza hitimisho lako: “ Jana suti yake mzuri iliashiria mafanikio yake. Ikiwa imechanika, ikifuka moshi, kuchafuka, leo suti yake iliyoharibika ilikuwa ishara ya anguko lake kutoka kwenye neema…“.
  • Washtue wasomaji wako kwa kuachana na ukawaida. Vunja muundo wa aya yako: “Jengo lililojengwa na Mark Mahela, hata kama lingekuwa imara zaidi, lisingeweza kuhimili...” 

CHEZA NA USHAIRI WA MANENO.

  • Linganisha vina.Fanya aya zako ziwe na mizani pale maudhui yanaporuhusu kwa ajili ya ulumbi kidogo: “Kisiwa cha marashi, chamvurugia mtu utashi…”
  • Ongeza ushairi kidogo kwenye utunzi wako.Jaribu mlingano, kwa kurudia sauti ile ile ya mwanzo,  au ulingano, kwa kurudia sauti ile ile ya irabu.
  • Usijali sana kama utakuwa kidogo unatumia lugha ya mtaani.Ongeza nahau na lugha ya mitaani kwenye habari zako za maisha ya siku hadi siku:  “Poa! Nasepa!” 

HABARI NZURI NI ILE AMBAYO INAMFURAHISHA MWANDISHI WAKE KAMA AMBAVYO HUFANYA KWA WASOMAJI WAKE.