MASWALI YA MSINGI, MAJIBU YA MSINGI
Jukumu la msingi la mwandishi wa habari ni kumpa msomaji majibu ya maswali yaliyoko katika kinywa cha kila mtu pale jambo linapotokea. Kila mara maswali hayo ni yale yale na mara zote yanahitaji majibu yale yale. Miundo ya msingi ya uandishi wa habari inatofautiana tu kulingana na idadi ya vipengele vya majibu.
KUHABARISHA NI KUTOA MAELEZO
Daima kuna maswali makuu manne: Nani? Nini? Wapi? Lini? Jibu la mwandishi wa habari ni la msingi kama yalivyo maswali yenyewe. Linahusisha sentensi inayoelezea mhusika (nani?), kitenzi (nini?), eneo tajwa kulingana na mazingira (wapi?) na muda tajwa kulingana na mazingira (lini?). Mfano: Mark Mahela atekwa nyara kwenye makao makuu ya Benki ya Wafanyakazi jana usiku.
SIMULIZI NI KUTOA MAELEZO KWA KUELEZEA HABARI.
Kwa Ufupi ni muundo unaotoa habari kwa maelezo machache. Taarifa moja inatosha: Mark Mehela, mtaalamu wa masuala ya benki ambaye ni mkuu wa Benki ya Wafanyakazi, alitekwa nyara yapata saa 1:30 jana usiku kwenye makao makuu ya shirika hilo, yaliyoko Mtaa wa Ngawira. Watekaji wake, ambao walikuwa na silaha na kuvaa vinyago, walilipwa fidia ya shilingi milioni themanini kabla ya kutoweka kwa helikopta iliyokuwa ikingojea kwenye paa la jengo hilo. Mark Mahela aliachiwa, akiwa na kiwewe, lakini hakudhurika.
Aina hii ya kutoa habari inahitaji kiwango kikubwa sana cha urahisi wakati wa kuandika. Dondoo: epuka vielezi na vivumishi.
Simulizi ndiyo muundo unaotoa kiasi kikubwa zaidi cha maelezo. Haya ni maelezo ya kina ya tukio kama lilivyotokea ambayo yanaunganishwa na tukio jingine kwa mtiririko au mantiki kumjulisha msomaji kile tunachokijua kuhusu tukio kwa usahihi iwezekanavyo. Mwandishi wa habari anachohitaji ni kuongeza tu maelezo ya msingi. Benki ya Wafanyakazi kwenye Mtaa wa Ngawira ilikuwa ikijiandaa kufunga milango yake jana usiku wakati watu wawili waliovaa vinyago na kubeba silaha walipovamia ukumbi wa jengo hilo ambao haukuwa na watu. Wavamizi hao wawili mara moja walienda hadi kwenye ofisi ya Mark Mahela iliyoko ghorofa ya nne ya jengo hilo. Kulingana na muda, kulikuwa bado na wafanyakazi wachache sana ofisini. Mark Mahela kwanza alifungwa kamba kwenye kiti chake, nk.
Namna zote za simulizi zinaangukia katika aina hii: taarifa , usimuliaji wa kawaida wa matukio mbalimbali na uhabarishaji wa matukio.
KURIPOTI NI KUTOA MAELEZO KWA NJIA YA UFAFANUZI
Ripoti ndiyo muundo unaotoa maelezo ya kina. Ni Simulizi inayoendana na ufafanuzi wa matukio yanayoripotiwa. Ufafanuzi huo unaongeza maelezo yote muhimu ya simulizi: kuipamba, sauti, hisia, visa vya kufurahisha, visa vya kutisha, nk. Ripoti zinamwezesha msomaji kujenga picha kichwani mwake mwenyewe. Matumizi ya vielezi, vivumishi na vitu vinavyoonekana na kusikika hufanya matukio kuwa halisi zaidi.
Mark Mahela, mtaalamu mashuhuri wa masuala ya benki, alikuwa mhanga wa tukio lisiloaminika la utekaji nyara jana usiku kwenye makao makuu ya Benki ya wafanyakazi, ambayo anaiongoza. Alikuwa akijiandaa kuvaa koti lake kurejea nyumbani yapata saa 1:30 usiku, wakati watu wawili, nyuso zao zikiwa zimefichwa kwa vinyago nyeusi, walivamia ofisi yake kubwa iliyoko ghorofa ya nne ya jengo hilo, huku wakiangusha maua yote yaliyokuwa kwenye vyungu vyake. Kulingana na katibu muhtasi wa Mark Mahela, ambaye alishuhudia matukio yote, wateka nyara hao waliingia ofisini humo taratibu kabla ya kupaza sauti: “Weka mikono juu! Haraka!”
Haijalishi habari hiyo ni ndefu kiasi gani, ufafanuzi ni sehemu ya ripoti.
MASWALI YA ZIADA, MAJIBU YA ZIADA
Kulingana na matukio yaliyotokea, wakati mwingine kuna maswali mawili ya ziada. Jinsi gani? Kwa nini? Mswali haya huulizwa pale matukio yanaposhindwa kueleweka mara moja. Ili kuhakikisha kwamba wanaweza kueleweka vizuri zaidi, mwandishi wa habari huongeza ufafanuzi fulani wakati anapoweka habari hiyo kwenye maandishi.
KUHABARISHA NI KUELEZEA
Kutoa majibu ya “jinsi gani” na “kwa nini” ya matukio yanayoongelewa inamaana kuelezea chimbuko, kishawishi na sababu za matukio hayo. Inamaanisha kuyachunguza matukio hayo kwa karibu zaidi, kwa umakini zaidi, kwenda mbali zaidi ya kinachoonekana machoni kuchanganua uasili na kusimbua maana yake halisi.
KUCHUNGUZA NI KUELEZEA WAKATI WA UKIFANYA UCHAMBUZI
Uchunguzi ni muundo wa maelezo ya kina na uchambuzi. Hufanya mambo kueleweka. Huhusisha kunyambua matukio katika vipengele vyake. Je, Mark Mahela alitekwa jana usiku? Mwandishi wa habari za uchunguzi anakusanya data zote zilizopo na kisha anaelezea nini yalikuwa madhumuni ya wateka nyara na pengine, hata ni namna gani walivyojiandaa kumteka nyara, ni madhara gani tukio hilo linaweza kuwa nayo kwa benki, nk. Kazi hii ya uchambuzi huhitaji uelewa wa mada husika, nyaraka sahihi, vyanzo vya kuaminika, taarifa sahihi za mashahidi na muda wa kufikiri. Wakati mwingine inatokea kwamba uchunguzi wa kichambuzi unashindwa kuelezea mambo fulani kutokana na data kutoonekana, kufichwa au kuzuiwa. Katika matukio kama hayo, mwandishi wa habari huanza kufanya utafiti nje ya data zinazofahamika. Huu ndiyo uchunguzi, muundo wa kina zaidi wa kutoa habari.
KUHOJI NI KUELEZEA WAKATI UKIFANYA UCHAMBUZI
Mahojiano ni mchakato wa kichambuzi unaohusisha mabadiliko. Pale mwandishi wa habari anaposhindwa kutoa maelezo anayotegemewa kuwa nayo, basi hutafuta ushauri wa mtaalamu kwenye eneo hilo. Mark Mahela amekuwa mhanga wa kutekwa nyara! Bwana Maridadi, wewe unaielewa vyema Benki ya Wafanyakazi, unaweza kuelezea nini yanaweza kuwa madhara ya tukio hili kwa benki hii?… Mahojiano yanayochapishwa kwa muundo wa maswali na majibu ndiyo hasa huelimisha zaidi.
KUHABARISHA NI KUTOA TAFSIRI
Pale simulizi, ufafanuzi na uchambuzi unaposhindwa kutoa majibu ya matukio yanayoongelewa, mwandishi wa habari anaweza kutafsiri ukweli: ikiwa hawezi kupata maelezo kamili ya ukweli, basi atajaribu kuyasimbua kwa kutumia vidokezo kidogo vya habari alivyonavyo.
KUTOA MAONI NI KUTAFSIRI WAKATI UKIFANYA TATHMINI
Kuna namna kadhaa ambazo waandishi wa habari wanaweza kushirikisha mawazo yao binafsi kwa wasomaji wao, lakini yote ni aina za maoni ya mhariri: makala za maoni, makala za maoni binafsi, michoro: Mark Mahela alitekwa jana usiku, saa chache tu baada ya kuwatangazia wafanyakazi wake mpango wa kupunguza idadi kubwa ya wafanyakazi. Ni vigumu kuamini kwamba matukio haya mawili hayahusiani… Ni juu ya msomaji kuamua usahihi wa tafsiri hiyo.
MAONI BINAFSI NI KUTAFSIRI WAKATI UKITOA MSIMAMO
Ikiwa, mwishoni mwa tafakuri yake binafsi, mwandishi wa habari atafikia uamuzi wa kimaadili kuhusiana na matukio ambayo ameyaongelea, ameyachambua na kuyachunguza, basi atakuwa anaandika maoni yake: Kutekwa kwa Mark Mahela kutachelewesha kupunguza wafanyakazi. Msomaji yuko huru kuchagua iwapo atakubaliana na mtizamo huu au la, ambao, katika tukio lolote, linaangazia mchakato wa fikra za mwandishi wa maoni hayo na hivyo kuwa sehemu ya habari yenyewe.