Menu

10. Kupiga na kuhariri video ya mtandaoni

Kufuatia ujio wa simu za kiganjani na upatikanaji kirahisi wa vifaa vya kitaalamu vya kutengeneza filamu, mapinduzi aina mbili yameendelea kwa wakati mmoja katika midia: video imekuwa moja ya njia kuu zaidi za kusambaza habari mtandaoni na utengenezaji wa maudhui umerahisishwa sana.

Nini jukumu la sasa la video mtandaoni?

Tukichukua aina zote za midia na kuziweka pamoja (habari na burudani), sasa video inachukua zaidi ya robo tatu ya matumizi yote ya intaneti duniani. Katika kipindi cha miaka kumi au zaidi kidogo, kutokana na kuongezeka majukwaa ya kutiririsha video, tovuti za kuhifadhi maudhui kama YouTube, pamoja na matumizi makubwa ya simu za kiganjani, video zimechukua kabisa nafasi ya maandishi katika kusambaza habari mtandaoni.

Kulingana na midia, hii imewezesha kuibuka kwa aina mpya ya usimuliaji habari, kama inavyooneshwa na mafanikio ya Brut. Taratibu, vyumba vyote vya habari vimewekeza katika kutengeneza maudhui kwa ajili ya tovuti na akaunti zao za mitandao ya kijamii. Hilo ni sahihi kwa magazeti ya kitaifa na yale ya kila siku ya kikanda.

Ni vifaa gani vinaweza kutumika?

Siku hizi, kuna vifaa vichache ambavyo havikuwezeshi kuandaa maudhui yenye ubora. Yumkini unaweza kupendelea zaidi kupiga filamu kwa kamera ya kawaida (aina ya 5D), lakini ukweli ni kwamba simu yako ya kiganjani tayari inatoa picha za ubora wa hali ya juu kwamba si tatizo kuziweka mtandaoni.

Ukitaka kutumia iPhone yako, kwa mfano, wabobezi wanapendekeza kwamba angalau utumie iPhone 6 plus. Kwa kukukumbusha tu, kifaa hicho kilitolewa mwaka 2014. Bila shaka, simu za kiganjani siku hizi zinatosha kabisa kwa kuandaa ripoti fupi. Hata hivyo, ikiwa unapanga kutengeneza video ndefu sana itakuwa rahisi zaidi na bora zaidi kupiga picha kwa kutumia vifaa maalum.

Kuhariri kwenye simu ya kiganjani au kwenye kompyuta?

Kinachofaa kwa kupiga picha kinafaa pia kwa kuhariri. Ikiwa unataka kuandaa ripoti fupi kwa ajili ya tovuti yenu ya habari au akaunti zenu za mitandao ya kijamii, simu ya kiganjani inatosha. Kuna programu kadhaa zilizotengenezwa mahsusi kwa madhumuni hayo. Kwa mfano, Filmic Pro na Kinemaster zote ni zana bora kabisa kwa simu yako ya kiganjani, kwa kuchukua video na kuhariri, kwa mfuatano huo.

Hata hivyo, ukitaka kutengeneza maudhui yenye ubora wa hali ya juu na marefu, kuweka nakshi na vipande vya mwendelezo, nk., kukaa chini na kuanza kuhariri video yako siku zote itakuwa jambo zuri zaidi.