Menu

06. Kuandika ili kusomeka: namna ya kuziteka injini tafuti

Wakati vyombo vya habari vya kijadi vina namna yake ya kusambaza habari, tovuti za habari kimsingi vimeachana na hilo na kugeukia injini tafuti, Google ikiongoza. Injini tafuti hizi zinaweza kufananishwa na meza za kuuzia magazeti: ukitaka habari yako isomwe, lazima ipatikane huko. Kuna mbinu chache zinazoweza kukusaidia kufanikisha hilo.

Injini tafuti zinafanyaje kazi?

Injini tafuti ni roboti la mtandaoni. Kazi yake ni kutambaza mamilioni ya kurasa kila sekunde na kuzipa kiwango cha umuhimu kulingana na kile kilichomo ndani yake. Dhumuni ni kuhakikisha kwamba pale mwanadamu anapoweka neno-msingi kwenye upau wa utafutaji, roboti hilo linaweza kupendekeza kurasa zinazoendana zaidi na utafutaji huo.

Jukumu lako kama mwandishi wa habari ni kufanya iwe rahisi kwa mashine kuipata habari yako. Tatizo ni kwamba namna injini tafuti zinavyofanya kazi kwa ujumla haieleweki sana. Watengenezaji wake kamwe hawaelezi kwa ufasaha namna zinavyofanya kazi na hilo ni jambo la kawaida, kwa vile hiyo ndiyo kama siri ya kazi yao.

Faniboresho ya Injini Tafuti, inahusu nini hasa?

Kutokana na uzoefu, hasa katika Google, wachapishaji wa maudhui taratibu walielewa kwamba vipengele fulani ni muhimu kwa maudhui husika kutambazwa vyema na injini tafuti. Hii ndiyo maana ya Faniboresho ya Injini Tafuti (SEO).

Kuna vipengele takribani sita ambavyo ni lazima viwepo katika maudhui yako yote:

  • kichwa cha habari (kinaweza kuwa kirefu)
  • kidokezo
  • vichwa vidogo vya habari
  • picha na maelezo yake
  • viungo-wavuti vinavyoelekeza kwenye vyanzo vya kuaminika (vyombo vya habari, tovuti rasmi, nk.)
  • herufi 400 za kwanza za maudhui yako, ambazo lazima zijumuishe maneno-msingi yanayohusiana na habari yako.

Angalizo: maroboti (bado) hayatambui utani

Katika habari ya mtandaoni, unapaswa kuepuka kutumia kejeli na tungo tata, hasa kwenye vichwa vya habari na vichwa vidogo vya habari, kwa vile hilo litayadanganya maroboti yanayotambaza kurasa zako. Kwa hiyo, namna yoyote ile ya kucheza na maneno, majina ya utani na semi za kitadamuni zinazoweza kutumika katika aina nyingine za vyombo vya habari zinapaswa kuepukwa.