Menu

03. Jinsi ya kufanya utafutaji fanisi kwenye Google

Kufanya utafutaji mtandaoni ni rahisi. Hata hivyo, kupata kile hasa unachokitaka si rahisi sana. Kwa ujumla, unaweza kupata habari yoyote unayoitaka mtandaoni, na hivi hapa ni vidokezo kukusaidia uipate kwa urahisi na haraka zidi.

Msaada wa “Boolean operators” kwenye Google

Google ni zana muhimu sana, lakini jambo la msingi ni kwamba ni mashine tu. Na ili mashine ikufanyie kazi, unahitaji kujua inavyofanya kazi. Ukiandika JOHN MAGUFULI kwenye upau wa utafutaji, Google itakuletea orodha ya tovuti ambazo maneno JOHN na MAGUFULI yanapatikana. Kiuhalisia, injini tafuti inabadilisha uwazi kati ya maneno kuwa NA.

Sasa, ukiandika “JOHN MAGUFULI” (kwa alama za nukuu), Google itaelewa kwamba huwatafuti JOHN na MAGUFULI, bali JOHN MAGUFULI. Kwa mfano huu, matokeo ya utafutaji hayatakuwa tofauti sana, lakini hilo mara nyingi lina ufanisi zaidi.

Sasa, ukiandika -JOHN MAGUFULI (ukiwa umeweka – kabla ya JOHN bila ya kuacha nafasi), Google safari hii itakupa tovuti zote ambapo neno MAGUFULI linapatikana na JOHN halipo. Umeilekeza Google kuondoa neno JOHN kutoka kwenye utafutaji. Hii ni mbinu nzuri sana unapotumia maneno yanayofanana (homonyms).

Google Dorking

Mifano hii ya mwisho ndiyo kinachojulikana kama “Boolean operators”. Kutumia injini tafuti kwa namna hii hujulikana kama Google Dorking, kwa wale wanaojua mambo. Lakini hilo si mwisho. Injini tafuti inakuwezesha kutumia zana nyingine kuboresha utafutaji wako.

Ukiandika SITE: kwenye upau wa utafutaji na kisha kuongeza jina la tovuti mahsusi, Google itakuonesha tu matokeo kutoka kurasa za jina la tovuti hiyo. Kwa mfano, ukiandika SITE:habarileo.co.tz “JOHN MAGUFULI” (bila ya kuacha nafasi kati ya site: na habarileo.co.tz na kuweka JOHN MAGUFULI kwenye alama za nukuu), Google itakuonesha tu kurasa za tovuti ya gazeti la Habari Leo zenye maneno JOHN MAGUFULI.

Aidha, unaweza kutumia zana ya FILETYPE: (aina ya faili). Ukiandika hilo na kisha kuongeza kiendelezi (extension) cha aina ya faili, Google itakuletea tu kurasa zenye aina hiyo ya faili. Ukiandika FILETYPE:PDF, utapata tu kurasa zenye mafaili ya PDF. Hata hivyo, inapaswa kuzingatiwa kwamba zana hii inafanya kazi kwa aina chache tu za mafaili: mafaili ya maandishi yenye kiendelezi doc, mafaili ya lahajedwali (spreadsheet) yenye  kiendelezi xls na mafaili ya picha yenye kiendelezi jpg.

Sasa kwa kuwa umeyajua yote hayo, nitakuacha ujaribu matokeo ya utafutaji ufuatao: site:tanzania.go.tz filetype:pdf “bajeti”. Kisha Google itakuletea kurasa za kwenye tovuti ya serikali ya Tanzania, ambazo zina nyaraka za PDF zenye neno BAJETI. Matokeo yanaweza kuwa na mambo machache yasiyotarajiwa.

Usisahau kutumia zana ya utafutaji kulingana na muda

Kipengele cha mwisho cha kutosahau wakati wa kufanya utafutaji  kwenye Google ni zana ya kuweka muda. Unapofanya utafutaji kwenye ukurasa wa matokeo, chini ya kisanduku cha maandishi kuna orodha ya aina za matokeo (video, picha, ramani, habari, nk.). Kwenye upande wa kulia wa orodha hii, utaona kitufe cha “Zana” na, ukikibonyeza, menyu ndogo itatokea.

Bila shaka, zana muhimu zaidi katika menyu hii ni ile iliyo chini ya menyu kunjuzi ya “Wakati wowote”. Kwa kurekebisha mipangilio hii, utaweza kuiambia injini tafuti kukuonesha matokeo ya karibuni zaidi kuliko yale uliyoyapata awali. Unaweza pia kuainisha kipindi maalum cha muda. Hilo ni chaguo linalokupa ufanisi sana ikiwa unajua maudhui unayoyatafuta yalichapishwa lini.