Menu

20. Kulinda data na vyanzo vya habari

Mtandaoni, kama ilivyo maishani, mwandishi wa habari lazima aweze kulinda vyanzo vyake vya habari. Katika zama hizi za wadukuaji, ni muhimu kujua jinsi ya kuficha nyendo zako kwenye intaneti ili kuepuka kufuatiliwa, kazi inayofanana kidogo na mpelelezi anayehakikisha hafuatiliwi.

Kuwasiliana kwa usalama

Bila kumung’unya maneno, kamwe hutakuwa salama unapowasiliana na chanzo cha habari kama ambavyo ungekuwa endapo mtakutana ana kwa ana bila ya kuwepo kifaa cha kielektroniki. Mawasiliano ya awali ni nadra kufanyika kwa namna hiyo. Ukifanya kazi katika ulimwengu wa habari za kichunguzi, unaweza basi kulazimika kupata ufunguo wa PGP ambao utakuwezesha kusimbafiche (encrypt) mazungumzo yenu. Unaweza pia kuchagua kutumia mifumo iliyoandaliwa tayari kama vile akaunti za barua pepe za ProtonMail.

Kuperuzi intaneti bila kujulikana

Kuperuzi kwa siri mtandaoni pia ina maana kutoacha alama za nyendo zako. Kila kompyuta duniani ina “utambulisho” wake, unaojulikana kama anwani ya IP. Unapounganishwa na seva zinzohifadhi tovuti unaacha alama za nyendo zako.

Kwa hiyo, inaweza kuwa vyema kuficha anwani yako ya IP ili uweze kuperuzi bila kujulikana. Zana bora zaidi za kufanya hivi ni VPN. Hizi ni programu unazoziweka kwenye kompyuta yako zinazokuwezesha kutumia “njia” salama kati ya kifaa chako na intaneti. Anwani ya IP inafichwa na data zako zinafanyiwa usimbajifiche.

VPn nyingi zinaweza pia kutumika kama seva mbadala 9proxy), ambazo hukuwezesha kuficha au kubadili eneo lako na kuperuzi mtandao bila kujulikana, popote ulipo.

Baadhi ya zana fanifu na salama

Kuperuzi kwa usalama mtandaoni ina maana pia kuheshimu kanuni za msingi za usalama wa kidijitali. Kutofautisha nywila zako, kuzifanya ziwe ngumu zaidi kwa kutumia herufi kubwa, nambari na alama za uakifishaji, huu ni ulinzi wa msingi. Isipokuwa kwamba kukumbuka nywila nyingi inaweza kuwa vigumu. Unaweza kutumia zana ya kuhifadhi nywila zako, kama vile LastPass, ili kukusaidia katika hilo.

Ukitaka kuhifadhi na kuchambua nyaraka nyeti mtandaoni, si vyema kutumia zana zilizozoeleka za kuhifadhi nyaraka za makampuni makubwa ya kidijitali. Zana inayojumuisha kila kitu ni OverviewDocs. Pamoja na kulinda nyaraka zako, inakuwezesha kuzipa namba, kuzifaili na kufanya utafutaji fanisi sana wa maandishi.

Mwisho, kwa wale wanaotaka kuwasiliana na vyanzo vya habari nyeti kila siku, ni muhimu kuepuka kutumia huduma zilizozoeleka za kutuma ujumbe mfupi. Katika eneo hili, Telegram na Signal ni zana zinazochukuliwa kuwa salama zaidi.