Menu

22. Kutengeneza “chapa binafsi”

Kinadharia, hakuna kanuni za “chapa binafsi”, ni zile zile zilizochukuliwa kutoka utafutaji masoko kuhusu kutengeneza chapa mtandaoni. Ukiwa mtaalamu wa habari, na si mtaalamu wa masoko, kanuni chache za hekima zinapaswa kutumika, hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Ni mijadala gani ifanyike kwenye mitandao ya kijamii? Binafsi au kitaaluma?

Wakati hakuna jambo linalokuzuia kufungua akaunti binafsi, hadhi yako katika jamii kama mwandishi wa habari ina maana kwamba unalazimika kuiangalia mitandao ya kijamii kwa mtizamo wa kitaaluma (ambao haukatazi kutuma jumbe binafsi). Hizi hapa ni kanuni chache za namna ya kuenenda kwenye mitandao ya kijamii (Facebook, Twitter na mingine):

  • Onesha kwamba wewe ni wewe, jambo linalomfanya mwandishi wa habari avutie
  • Onekana mahali na katika maoni ya viongozi ambapo “mambo yanatokea”
  • Tumia lugha binafsi na rahisi zaidi kuliko katika makala zako
  • Tenda kwa uwazi
  • Usiogope kusema “Sijui”
  • Usiogope kukubali “Nilikosea”
  • Usisite kuiomba jumuiya yako wakati ukitafuta taarifa
  • Usisahau kushukuru/kutamambua/kuunga mkono kile wataalamu wengine wanachofanya.

Hivyo, kutengeneza “chapa” yako kama mwandishi wa habari huhitaji kufanya kazi kubwa mwanzoni (kufuatilia na kuripoti habari na vyanzo husika) kama ilivyo mwishoni (kuifanya kazi yako ifahamike). Moja haiwezi kwenda bila ya nyenzake na utaungwa mkono na kuthaminiwa na watumiaji wa intaneti ikiwa utapata namna ya kuitumikia jumuiya yako. Usisahau kwamba intaneti, kwanza kabisa, ni eneo linalotawaliwa na falsafa ya kushirikishana.

Utaifahamishaje jumuiya yako kuhusu kile unachokifanya/kukichapisha?

Kwa kuwa mitandao ya kijamii kwanza kabisa ni maeneo ya kujieleza binafsi, ni jambo zuri kuifahamisha jumuiya yako unachokifanya. Tasnia mpya inategemea zaidi kuelezea kile kinachoendelea nyuma ya pazia: waandishi wa habari wanafanyaje kazi yao? Wanaenda wapi? Mbinu zao za uchunguzi ni zipi? Mada zote hizi zinawawezesha watumiaji wa intaneti kuelewa vyema jinsi habari inavyotafutwa.

Wasomaji wetu wanapenda kujua ikiwa tunashitakiwa kwa kashfa (na nani) au kwamba chanzo fulani cha habari hakitaki kujibu maswali yetu.

Ufahamu wa kile tunachochapisha ni wa kimapokeo zaidi. Katika hili pia, waandishi hawakusubiri hadi kuja kwa intaneti ili kufanya habari zao “ziwavutie” watu wengi zaidi. Kila mtu ana namna yake ya kufanya mambo, kulingana na haiba yake na utamaduni wa chombo chake cha habari. Gazeti la udaku kama vile The Sun halitakuwa na mbinu zile zile za “kujiuza” kwa wasomaji wake sawa na New York Review of Books!

Je, tunahitaji kuwa kanuni za utumiaji wa mitandao ya kijamii kwa waandishi wa habari?

Hili ni swali linalojirudia-rudia hivi leo, hasa tangu vyombo vya habari vikubwa vijipe maazimio na miongozo kuhusu jambo hilo. Kwa mantiki hiyo pia, uhusiano unaodumishwa na kila chombo cha habari hubainisha lugha yao wanayotumia kwenye mitandao ya kijamii. Utii kwa kampuni na kuheshimu kanuni zilizowekwa inaonekana kuwa jambo la busara. Walakini, waandishi wa habari hawakatazwi kutokubaliana na msimamo “rasmi” wa chombo chao cha habari kuhusu uandishi wa habari kwa sababu, kama inavyoeleweka vyema, inapokuja kwenye masuala nyeti, mara nyingi hakuna njia moja inayofaa na isiyopingika ya namna ya kuandika habari zake!