Menu

23. Zana za kuchambua watembeleaji wa tovuti

Kuendeleza tovuti yako, unahitaji kuijua hadhira yako: ni nani hao? Ni wakati gani hutembelea tovuti? Ni kurasa zipi wanazipenda zaidi? Haya ni maswali yote ambayo programu kadhaa sasa zinaweza kuyatolea majibu ya kina.

Zana

Kuna zana kadhaa zinazoweza kufanya uchambuzi wa hadhira ya tovuti, kwa maana ya idadi na ubora. Zana zinazojulikana zaidi ni pamoja na:

Chartbeat inatoa kipimo cha wakati halisi cha watembeleaji wa tovuti, tangu ukurasa wa mwanzo hadi kurasa mahsusi. Baadhi ya vyombo vya habari vinaitumia dhana hii kubaini habari zinazotizamwa zaidi. Pamoja na wanapotokea watumiaji na mahali wanapokwenda baada ya kutazama kurasa zako. Kasoro yake ni kwamba programu hii haipatikani bure.

Google Analytics inafanya karibia kazi ile ile, lakini kutoka siku moja hadi inayofuata na katika toleo liliogawanywa katika majedwali tofauti (hadhira, maudhui, vyanzo vya watembeleaji na matangazo). Kasoro ya Google Analytics ni kwamba haitofautishi watumiaji na badala yake inahesabu tu utembeleaji (ukitembelea tovuti hiyo hiyo kazini na nyumbani, itahesabu kama watembeleaji wawili tofauti) na kwa hiyo inaelekea kutoa idadi kubwa ya watembeleaji kuliko hali halisi.

Nielsen ni kampuni binafsi inayotoa idadi ya hadhira kulingana na taarifa inayotafutwa na watumiaji wa intaneti (na si watembeleaji halisi wa tovuti). Mbinu hii inatoa picha sahihi zaidi ya watembeleaji wa intaneti na ndiyo njia pekee inayotumiwa na wanaotoa matangazo ya bishara kubaini viwango vya tovuti. Kasoro ya Nielsen ni kwamba kwa kutumia urejeaji mzuri na tovuti “haramia” za kukusanya habari mbalimbali kutoka tovuti nyingine (tovuti za michezo, kwa mfano), ni rahisi sana kutengeneza muongezeko bandia wa watembeleaji wa tovuti.

Mbinu mbili za kawaida

Mbinu inayojulikana kama “site-centric” ina uwezo wa kuchambua kwa usahihi data muhimu ya watembeleaji tovuti, kwa vile inahesabu idadi ya “kuitwa” kwa ukurasa na kivinjari. Kipimo hicho huwezesha kubaini idadi ya kutembelewa na kutazamwa ukurasa. Kinatumika kwa intaneti ya kawaida na intaneti ya simu za kiganjani.

Mbinu inayojulikana kama “user-centric” inarekodi matumizi yote ya intaneti kwa idadi fulani ya watumiaji (paneli ya Nielsen, takribani watumiaji wa intaneti 25,000). Kipimo hiki kinawezesha kupata uelewa wa kina sana wa wasifu wa watumiaji wa intaneti na huwezesha ulinganifu wa viwango vya upenyaji wa tovuti mbalimbali; hata hivyo, hakihesabu watumiaji wa intaneti wanaojiunga kutokea muunganisho wa umma au ughaibuni.

Vipimo vikuu

Kwa sasa, kigezo cha kwanza cha idadi kwa ajili ya kutathmini tovuti ni watembeleaji wa kipekee (UV), yaani idadi ya watumiaji wa intaneti waliotazama moja ya kurasa za tovuti angalau mara moja katika mwezi uliopita. Tovuti ishirini bora za Uingereza zina watembeleaji wa kipekee milioni 2 hadi 10 kwa mwezi, wakati China, idadi hiyo ni ya siku moja tu… Idadi ya utembeleaji pia hukokotolewa kwa programu ya uchambuzi wa watembeleaji tovuti.

Kigezo cha pili ni utazamaji wa kurasa, yaani idadi ya kurasa zinazoitwa kila mwezi. Kinapima kiwango cha watembeleaji kwenye tovuti na, kwa hiyo, kiwango cha mvuto uliotokana na maudhui ya habari. Kwa mshangao, muda wa kila utembeleaji bado hauhesebabiwi na mashirika mbalimbali ya kupima watembeleaji tovuti yanayotumiwa na wanaotoa matangazo ya biashara, ingawa kigezo hiki ni kiashiria cha kutegemewa ya ubora wa maudhui ya habari na mapenzi yaliyooneshwa na watumiaji.

Mwisho, grafu za watembeleaji tovuti za habari zina sifa moja kwa kuwa zote zinaundwa na vilele vya hadhira viwili vyenye umbo la herufi M, asubuhi (saa 02:00 – 04:00) na nyingine jioni (11:00 – 01:00), wakati watu wakirejea nyumbani na baadhi kwenda kazini.