Menu

19. Kuandaa maelezo ya midia-anuai

Mtandaoni, hata maana ya habari ni tofauti na inavyoeleweka na midia nyingine. Tangu “Tweet” ndogo hadi uchambuzi wa kina, bahari ya mtandaoni ya midia-anuai ni mchakato wa maelezo unaobadilika na kukua kadri muda unavyoendelea na unahitaji kurejewa mara kwa mara na mwandishi wa habari.

Mtandaoni, habari kamwe haiishi

Intaneti ni aina ya midia isiyokoma na inayoendelea kuhabarisha muda wote. Tofauti na runinga na redio (ambazo pia ni aina ya midia zenye mfululizo wa matangazo), hakuna muda wa vipindi uliopangwa, bila shaka kwa sababu intaneti iliibuka katika zama za utandawazi, ambapo habari huendelea 24/7. Kiutendaji, hii ina maana kwamba habari inaweza kuchapishwa wakati wowote, kuanzia asubuhi hadi usiku. Si lazima “kuzuia” habari, hata kama kuna watumiaji wengi zaidi katika nyakati fulani kuliko nyingine.

Si jambo la ajabu kwa habari kuanza na kiungo kidogo kinachoelekeza katika “Tweet” ya herufi 140. Hivyo ndivyo ilivyokuwa wakati wa kifo cha Michael Jackson, tangazo la kwanza ambalo lilikuwa ujumbe uliowekwa kwenye Twitter na tovuti ya habari inayoongelea tu maisha ya watu maarufu:

“DHARURA — TMZ.com inatangaza kwamba Michael Jackson amepelekwa hospitali ya Los Angeles kufuatia tatizo la moyo”.

Ndani ya saa 24 baada ya “Tweet” hiyo, watumiaji wa Twitter waliongezeka maradufu na watumiaji wa Facebook waliongezeka mara tatu, ikiashiria nafasi iliyotumiwa kwa mazungumzo baada ya habari hiyo. Siku iliyofuata, magazeti makubwa duniani ya kila siku yaliweza kuandika wasifu wa kina wa marehemu kwa wasomaji wao. Miaka miwili baadae, daktari aliyemtibu mwanamuziki huyo maarufu saa chache kabla ya kifo chake alishitakiwa na kutiwa hatiani na mahakama ya Los Angeles. Habari hii ni mfano mzuri wa kuelezea dhana ya habari inayoendelea, ambapo maudhui huongezwa kadri jambo jipya linavyotokea, hata baada ya muda mrefu kupita.

Ni namna gani marekebisho yajumuishwe?

Moja ya changamoto za uandishi wa habari mtandaoni ni kufanya mabadiliko ya kudumu katika habari yaonekane na yawe na mguso. Kwa hiyo ni muhimu kuonesha tarehe (siku, mwezi, mwaka na muda wa kuchapisha) na ainisho (tag) hususa la maudhui, kwa vile hilo huwawezesha watumiaji wa mtandao kuitambua habari hiyo. Pia huboresha sana makumbusho yako. Kila mara habari ya kifo cha Michael Jackson itakapochukua umuhimu tena, maudhui hayo “yatarejelewa” na injini tafuti na kusomwa (au kusomwa tena) na watumiaji wa mtandao.

Katika muktadha kama huo, ni muhimu kwamba waandishi wa habari kuzingatia kanuni mbili:

  • kukiri kwamba kosa lilifanyika baada ya kuripotwa na mtumiaji wa intaneti, na
  • kulionesha kosa hilo, kwa kutoa masahihisho mwishoni mwa habari.

Kukubali kosa kutaongeza heshima unayopata kutoka kwa wasomaji na kutaongeza unyenyekevu wa waandishi wa habari wengine.